Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, amesema amefurahishwa na Kampuni kuzalisha mabomba ya maji nchini ya Plasco Ltd jinsi ilivyojipanga kuzalisha mabomba ya kisasa ya maji kwa ajili ya miradi ya maji inayaoendelea nchini.
Akizungumza juzi baada ya kutembelea kiwanda hicho kilichopo cha Chang’ombe Dar es Salaam na kujionea uzalishaji wa mabomba ya kisasa aina ya weholite yenye uwezo mkubwa ambayo hutumika katika miradi mikubwa maji safi na maji taka na miundombinu ya barabara.
Waziri Aweso amesema; “Nimefurahishwa jinsi kampuni yenu ilivyojipanga katika teknolojia ya kisasa ya utengenezaji mabomba, hapo awali sikujua kama mambo mazuri ya aina hii yapo hapa nchini, sasa nimeona na nipo tayari kushirikiana na yinyi kuhakikisha miradi yetu ya maji haikwami kwa kisingizio cha ukosefu wa mabomba.
“Kuanzia sasa sitarajii kusikia makandarasi wakisingizia ukosefu wa mabomba, kwamba ndiyo yanawakwamisha kukamilisha miradi,” amesema Aweso.
Waziri Aweso amesema hayo wakati wa ziara ya kutembelea wadau wa maji vikiwemo viwanda katika Mkoa wa Dar es Salaam na kusisitiza kuwa amejifunza vitu vingi.
“Nimejifunza vitu vingi na kuona umuhimu wa sisi Wizara na Serikali tunaweza kumaliza tatizo la maji kwa wananchi wetu kama kujenga ushirikiano wa karibu na kuaminiana.
“Baada ya kuzungumza na wadau sasa wizara yangu tunajipanga kuandaa mkutano wa pamoja wadau wa sekta ya maji, wataalamu na wizara zote ambazo ni washirika wetu tuzungumze kwa pamoja ili kuhakikisha tatizo la maji linaisha, kama alivyoelekeza Rais Dk. John Magufuli,” amesema Aweso.
Kwa upande wake Afisa Uendeshaji wa Kiwanda cha Plasco, Alimiya Osman, amesema wamefurahi kutembelewa na Waziri Aweso na Uongozi mzima wa RUWASA na DAWASA na kuahidi kuendelea kushiriana kwa ukaribu zaidi na wizara hiyo ili kuongeza ufanisi katika kazi zao.
“Sisi kwa upande wetu tumejipanga vizuri na wataalumu wetu kuhakikisha tunatumia teknologia ya kisasa tuliyo nayo katika uzalishaji kwa wakati mabomba yenye viwango vya kimataifa.
Source: Mtanzania.co.tz