Plasco Limited yaboresha teknolojia ya uzalishaji wa mabomba Tanzania

June 21, 2021
AllIn the Media

Kampuni ya Plasco Limited, wazalishaji wa mabomba ya maji imezindua muonekano wake mpya ‘Brand identity’ ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia katika uzalishaji wa bidhaa na huduma katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Uzinduzi huo umefanyika kwa kutumia kauli mbiu isemayo “We Stand for Quality” yaani tunasimamia ubora, ikidhihirisha uwezo wa kampuni hiyo katika kuzalisha bidhaa bora na zenye viwango vya kimataifa hapa nchini.

Muonekano huo mpya una akisi matumizi ya teknolojia ya kisasa zaidi kwenye uundaji wa vifaa na huduma zake.Pia, utaiwezesha kampuni kufikia malengo makubwa iliyojiwekea katika miaka ijayo.

Ikiwa imeanzishwa takribani miongo mitatu iliyopita, Plasco Limited ni kampuni inayoongoza katika utengenezaji wa mabomba ya plastiki ikizalisha mabomba aina mbalimbali ikiwamo unplasticized polyvinyl-chloride (uPVC), High Density Polyethylene (HDPE) pamoja na mabomba aina ya Weholite HDPE ambayo ni teknolojia ya kisasa zaidi.

Weholite ni mabomba ambayo Plasco Limited inatengeneza kwa kutumia teknolojia ya kisasa kutoka kampuni ya Uponor Infra Oy ya Finland, ambayo yana kipenyo kikubwa na ukuta mpana na yamethibitika kuwa suluhu ya muda mrefu kutokana na uwezo wake wa kudumu kwa zaidi ya miaka 100.

Ofisa Uendeshaji Mkuu wa Plasco Limited, Alimiya Osman alisema “Imekuwa safari ndefu ya kuijenga kampuni yetu na tumeamua kufanya mabadiliko kuendana na mageuzi ya teknolojia kwenye sekta hii.Tumejizatiti kuzalisha bidhaa bora na zenye viwango vya kimataifa ambazo zinaweza kudumu kwa muda mrefu.Hiyo ni sababu tumewekeza kwenye teknolojia ya Weholite ambayo ni ya kimataifa ambayo inatumika kwaajili ya ujenzi wa makalavati, miundombinu ya maji kama mitaro mikubwa, utunzaji wa maji na umwagiliaji,” alisema.

Aliongeza “Tunafurahi kwamba bidhaa zetu zote na huduma tunazotoa zina viwango vya hali ya juu na ndio maana tunazindua muonekano mpya kuonesha ni jinsi gani tunasimamia na kujali ubora wa bidhaa ‘We stand for Quality’. Taswira ya kampuni yetu ina akisi mambo ambayo tunataka kuyafikia kwenye sekta hii na tukiwa kama wauzaji wa bidhaa nje ya nchi, Plasco ni uthibitisho tosha kuwa kampuni za kitanzania zina miundombinu na uwezo wa kutoa bidhaa zenye viwango vya kimataifa katika ukanda wa Afrika Mashariki na zaidi,” alisema Osman.

Akizindua muonekano mpya wa Plasco kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (Tirdo) Prof Mkumbukwa Mtambo aliipongeza Kampuni ya Plasco Ltd kwa kubadili mwonekano wake ambao unaonyesha ufanisi wa teknolojia yake mpya ya kisasa, Weholite.

“Inatia moyo kuona Tanzania inakuwa nchi ya kwanza katika bara la Afrika na ya 11 duniani kuanzisha teknolojia ya Weholite. Teknolojia hiyo ni suluhisho la muda mrefu la changamoto za miundombinu ya maji safi na maji taka nchini,” alisema.

“Sekta binafsi ni usukani wa kuendesha na kuongoza uchumi wa viwanda Tanzania na Plasco imethibitisha hilo. Ili kuwa nchi ya viwanda, tunahitaji aina hii ya viwanda ambavyo huzingatia ubunifu katika kuleta ushindani endelevu,” aliongeza.

Aliishauri Kampuni ya Plasco Ltd kutafuta masoko mapya nje ya Tanzania ili kukuza uzalishaji na mtaji Pamoja na kuongeza ajira.

Prof Mtambo aliipongeza kampuni hiyo kwa kujenga maabara ya kupima ubora wa bidhaa ndani ya kiwanda hicho, tofauti na makampuni mengine ambayo hayazingatii kipengele hicho muhimu.

Source: Michuzi Blog